Pages

Sunday, January 6, 2013

Maji ni uhai

HIVI karibuni kumetokea uhaba mkubwa wa maji duniani. Kwa wale tuliozaliwa miaka ya sabini na kurudi nyuma tulishuhudia watoto wakiogelea katika mabwawa yaliyokuwa yamezagaa nchi nzima, mito ilikuwa imejaa mpaka watoto walikuwa wakizama na kufa maji, mabomba yalikuwa yakitoa maji safi na yenye uhakika kila nyumba kwa vile huko yalikokuwa yakitoka kulikuwa kuna chemchem zenye uhakika wa kutoa neema ya maji safi pia kwa wakazi wa vijijini.


Maji yanauzwa:
Nyumba za vijijini kama kawaida zilikuwa na mitungi mikubwa ya kuwekea maji na juu yake kuliwekwa kata ya kuchotea na kunywea maji hayo ambayo yalikuwa na harufu na ladha nzuri ya ajabu isiyoelezeka labda msomaji wangu unisaidie kuielezea. Lakini maji hayo pia yalipatikana kwa gharama ya kupiga hodi, kusalimia na kuomba maji ya kunywa tosha! Vivyo hivyo mijini nako mambo yalikuwa si haba, hakika iliwezekana pia kupiga hodi nyumba yoyote ukasalimia vizuri na kuomba maji ya kunywa na wakakuletea galoni la maji lenye umande toka katika friji pamoja na glasi ujisevie...
Lakini mambo leo hii yamebadilika. Ndiyo, maji yanauzwa! Si kiyama hiki jamani? Kiyama kwa maana maji ndio uhai wa binadamu sasa uhai unauzwa shilingi ngapi? Yanauzwa! kwenye chupa haya, kwenye mifuko ya plastiki ambayo bila adabu yamepewa jina "maji ya viroba" haya, ya kupimiana kwenye glasi tuambukizane maradhi haya. Yanauzwa...
Maji ya chupa:
Lakini, hebu tuyaangalie kwanza maji haya yanayoitwa ya chupa jinsi yanavyopewa urasmi katika matumizi kwa mipango ya "lifestyle..." Hapana, japo ninaweza nikagusa maslahi ya watengenezaji wa maji ya chupa nchini kwa hili nitawaomba waniwie radhi maana wanywaji ni sisi raia tusiojua kitu na kuwapa wao maisha yetu kirehani-rehani tu. Tabia imejengeka tena ya kukereketa kabisa rohoni kuona watu eti wananunua lundo la maji ya chupa na kuyaweka majumbani familia ipate maji ya kisasa zaidi. Wengine ndio imekuwa kawaida kuzunguka na maji hayo kutishia wenzao kuwa wao hunywa kilicho bora, mambo yao safi.
Maji yaliyofungiwa kitaalamu ni maji maiti. Maji maiti kwa maana maji ni kitiririka na hupoteza maana halisi auhufa mara tu yanapokatazwa kutiririka. Hii inajulikana dunia nzima. Kwa kutambua hilo ndio maana maji yaliyofungiwa huwa yanaharibika yakikaa muda fulani (Expire date) hii inahitaji macho tu kuisoma katika chupa ya maji yoyote. Hivyo kwa kuwa maji yakifungiwa hufa, ndio maana unashauriwa kuyarudishia uhai kiujanja kwa kuyaweka katika ubaridi kabla ya kuyanywa. Na kwa kuhakikisha hilo hebu kunywa maji ya chupa ya moto uisikie ladha yake ilivyokufa. Hapa sisemi kuwa maji ya chupa hayafai, ila najaribu kukufahamisha msomaji wangu kuwa maji ya chupa si rasmi kwa matumizi bali ni msaada tu pale maji rasmi yanapokosekana. Wewe unatakiwa unywe maji hai tena ikibidi ukinge mdomo katika chemchem....
Maji ya Madimbwi:
Binadamu akishikwa na pilika za kiu huwezi kumzuia. Akina mama watakuwa mashahidi wangu wazuri maana kesi za watoto kunywa mafuta ya taa wakidhani ni maji wameshazizoea. Eneo fulani wanaweza wakawa na shida ya maji salama. Hawa wanaweza kuwa wana madimbwi na mifereji ya maji lakini wanayaogopa kuyanywa kwa kuwa yameshawapeleka ahera wengi na wengi wao pale wameshalazwa kwa kuambukizwa maradhi na vimelea vya maradhi vilivyomo mle.
Niliposhiriki "Route Match" na jeshi fulani hapa duniani nakumbuka nilifundishwa kuweka "Iodine pellets" ndani ya mkoba wangu kama kinga ya kunywa maji yoyote mbele yangu kwa kuwa tulitembea siku nane usiku na mchana ndio kikaeleweka. Iodine pellets kwa kiswahili ni "shabu" tena zipo tele masokoni na pengine madukani. hutataabika kuzipata na kama itakusumbua nitafute nikusaidie. Chukua punje moja tu yenye ukubwa wa kunde, tia katika glasi yako yenye maji, acha ikae kwa dakika tano hadi kumi kisha kunywa maji hayo. Utakuwa salama salimini.
Lakini angalia kuwa kunywa maji ya aina hii kunataka upelelezi mdogo kwa kutumia akili ya kawaida kabisa. Inakubidi kwanza kabisa kabla hujafanya chochote chunguza vyanzo vya dimbwi ua mfereji huo kama unatoka kwenye viwanda au makazi ya binadamu? Siri yako msomaji wangu, viwanda na binadamu ni wazalishaji wakubwa wa sumu zisizojulikana hivyo ukigundua vyanzo ni hivyo USINYWE maji hayo.
Maji yenye chumvi:
Kwa wakazi wa Jiji la Dar Es Salaam hasa maeneo ya Mbagala wanayajua sana maji haya. Wao wanayapata toka katika visima vilivyozagaa maeneo hayo maana ndivyo vyanzo vyao vikubwa vya maji wanayotumia. Maji chumvi kitaalamu si maji salama japo unaweza ukayapata yakiwa safi. Usalama wake si wa kuaminika kwa kuwa ardhi ina utajiri wa madini ya aina nyingi zenye tija kwa binadamu lakini ardhi inabeba pia madini yenye sumu baridi (slow killer agents) ambayo unaweza kuyaonja katika maji na kusema ni "chumvi" bila kujua ni chumvi gani, na kama ni sumu au la.
Kisima kinachotoa maji yenye sumu baridi za aina hii hudhoofisha afya za wakazi wanaolizunguka eneo hilo kila wanapoyatumia maji hayo na siku moja sumu ikiwakolea ndipo mnakutana hospitali wakazi wa mtaa mzima bila kumjua mchawi wenu na huku dakitari akijikuta haujui ugonjwa wenu pia... Mtajikuta mmefanana na wakazi wa mji fulani waliokula nyama toka bucha moja ambalo bila kujua muuza bucha alikuwa anakatia nyama katika gogo la mti wenye asili ya sumu baridi. Ugonjwa wa ajabu mtaa mzima! Walijikuta mtaa mzima wamejaa hospitali, hawajulikani wanaumwa nini..... Tutaizungumza mungu akipenda.
Lakini msomaji wangu siwezi kukuacha yakukute. Unajua kuitenganisha chumvi na maji ya kunywa ni shughuli kubwa, yenye mipango mingi pengine kufungua kiwanda. Hapa ninayo mbinu ya kijeshi na ya kisayansi zaidi unayoweza kujichujia chumvi hiyo na ukapata maji japo kidogo ya kunywa. Fanya hivi: Chukua beseni tia maji hayo haramu yenye chumvi nenda kaweke juani.
Chukua jagi au kikombe kizito kisichoelea weka katikati ya beseni lako lakini angalia maji yasizidi yakaingia kwenye chombo chako na uhakikis ` he chombo hicho hakielei kimetuama kabisa. Chukua karatasi la nailoni ziba juu ya beseni lako kisha funga na kamba ikaze beseni lizibe kabisa. Chukua jiwe dogo saizi ya ndimu weka katikati ya karatasi pale juu ili lilete kauzito fulani.Pamoja na kauzito hako angalia karatasi lisikiguse chombo ulichoweka ndani.
Subiri maji yajichuje, baada ya masaa matatu nenda kafunue karatasi. Utakuta maji yenye chumvi ndani ya beseni yamekuwa ya moto yanatoa mvuke ambao unatengeneza umande kwenye karatasi la nailoni kwa ndani. Sasa, kwa kuwa nje umeweka jiwe katikati, basi umande ule pale ndani utatiririka kuja kati kwenye uzito na kisha ni kuangukia kwenye chombo kitupu ulichokitega kwa ndani. Utakapofungua lile karatasi utakuta chombo chako kina maji na ukiyanywa ni bariiidi kabisa hayana chumvi. Unaweza ukatengeneza chombo kikubwa zaidi kama matumizi yako ni makubwa ila utatakiwa kujua namna ya kupiga hesabu za kifundi. Ukishindwa niite nikusaidie.
Maji ni nini?
Maji ni neema ya kiuumbaji tuliyopewa na mola wetu bure! Shika hilo maana ukituuliza wanasayansi tutakuambia maji ni molekule yenye atomi mbili za haidrojeni na atomi moja ya oxygen. Molekule hizo ndizo zinazounda kitu kiitwacho maji. Hakuna kitu muhimu duniani kama kunywa maji. Lakini kunywa maji safi na salama ndio busara ya kawaida kwa kila mtu. Maji hupatikana toka katika chemchem, mvua na vyanzo vingine vingi tu kama vile maji madini ya visima virefu nk. Umuhimu wa maji kwa binadamu ni mkubwa kupita maelezo kiasi kwamba wataalamu wa afya wa aina zote duniani wamekiri kuwa maji ndio uhai. Unaweza ukanywa, ukaoga, ukapikia, ukaoshea, ukanyweshea n.k. lakini usisahau shughuli za kiroho kama kubatiza, kusilimisha, kutibu, kuapisha na hata ukija kwangu nitakutibu kwa maji tu! ndiyo, nina ibada ya kuomba chochote kiwe mwilini mwako kwa maji na ukapona.
Kwa nini unywe maji?
Kuna tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa mtu aliyekunywa lita mbili za maji au glasi nane tu kwa siku alitupa dawa za maumivu ya viungo baada ya wiki mbili tu. Mwingine alitupa dawa za kizunguzungu na kuumwa kichwa. Wapo pia waliopona bila kujijua maradhi ya aina nyingi sana. Hebu tujiulize maji huwa yanaenda wapi mwilini?
Kwa ujumla binadamu yeyote ni maji kwa 55% hadi 78% kulingana na ukubwa wa umbo lako. Labda nikuambie kuwa maji ni theluthi mbili ya mwili wa binadamu yeyote yule aliye hai hivyo ndio maana watu wakiamua kukuua hukuchinja. Wanakata mshipa mkubwa ubebao maji yote ya mwili pale shingoni na ukikauka maji umetuaga!
75% ya misuli ya binadamu ni maji
 Mtu asiyekunywa maji hana nguvu, amini kabisa. Kama vipi jiulize mbona mtu akiwa mgonjwa taabani huomba maji na si kinginecho. Umewaona wauguzi wajanja? Kabla ya yote mgonjwa anapewa dripu za maji kwanza. Shangaa...
90% ya ubongo wa binadamu ni maji.
Maji katika ubongo humfanya mtu awe na uwanja mpana mno kifikra katika kufikiri, kutoa maamuzi, kukiri, kusamehe, kushauri na kila kitu kiitwacho fikra sahihi. Alama ya kwanza kwa mtu asiyekunywa maji ni ubishi. Ukiona mtu anakuwa mbishi bila msingi basi mthibitishe kwa kumwangalia sura yake utagundua ni mzee kuliko umri wake... Maji. Ukimsogelea usoni mdomo wake unanuka vyakula vimevunda tumboni, huyo hanywi maji. Jichunguze msomaji wangu. Wewe si kikwazo kwa ubishi kwa wenzio? Kama vipi, kunywa maji.
22% ya mifupa ya binadamu ni maji.
Wazee mliofikia umri wa miaka 50 na kuendelea hebu nawaomba msogee mbele huku. Hapa nawaomba mnisikilize maana nyinyi ndio walalamishi mno wa maradhi ya mifupa lakini kunywa maji hamjui kuwa ni dawa. Ukinywa glasi 8 za maji kila siku kwa wiki mbili tu utanipigia simu kuwa maumivu yameanza kupungua. na ukiendelea kunywa maji kwa miezi mitatu utakuwa umepona sio tu mgongo, miguu, nyayo, kiuno, kizunguzungu na mengineyo, bali hata ujana unarudi! Niamini kabisa uone maajabu.
83% ya damu ya binadamu ni maji.
Hili sina haja sana ya kulijadili tena maana nimelisema hapo mwanzo na nafikiri hata wewe msomaji wangu tutakubaliana tu katika hili hata uwe mtoto mdogo. Usipokunywa maji unauakaribia mstari wa kupungukiwa na damu. Utakaribisha pia maradhi ya moyo kwa vivunde vya unavyokula bila kuviyeyusha na maji vinakuwa sumu kali mwilini na mwisho utakufa
Kazi za maji mwilini:
Maji yana kazi nyingi mno mwilini, na hata hivyo nyingi bado hazijawekwa bayana bado mpaka leo lakini nakupa tu hizi chache ambazo zinatosha kabisa kukushawishi msomaji wangu kuwa mnywaji mzuri wa maji. Maji yanasafirisha virutubisho vyote tunavyokula pamoja na hewa ya oksijeni kwenda sehemu zote za mwili. Maji ndio yanayoirutubisha hewa ya oksijeni katika mapafu, huku yakiwa bado kama korokorokoni kulinda na kukarabati seli zote za mwili.
Ukisikia mtu anasema kichwa kinauma mara kwa mara basi huyo hanywi maji! sio kichwa tu kinachouma pale, hata ngozi ya midomo inabanduka kwa ukavu, ni mwoga, hajiamini n.k. Maji pia hurekebisha joto la mwili, na ndio maana wakati wa jua wauza maji baridi ni neema kwao na wakati wa baridi wauza kahawa nao si haba... Lakini ukinywa maji basi ujue hayataishia mwilini bali yataenda kuchukua nafasi ya yale yaliyotumika na ndio maana ukiuonja mkojo una ladha kali lakini maji ulikunywa yakiwa matamu.
Shangaa. Kabla ya maabara duniani kisukari kilipimwa kwa dokta kuuonja mkojo wa mgonjwa ili aubaini ugonjwa! Upo ushahidi wa kumtibu mgonjwa wa maleria kwa kumpa maji kwa masaa kadhaa tu na akapona. Wazee narudia tena, mgongo, kiuno, miguu, usingizi, na shida zote za uzee kunywa maji glasi nane kila siku kwa wiki mbili uone maajabu! Elewa kuwa, hakika hakuna kisichotegemea maji toka unywele hata kufika miguuni kwenye ukucha wako.
Faida za maji mwilini:
Ukinywa maji utajisikia mwepesi maana yanavunja lehemu na sumu na kuzitolea kwenye mkojo. Ukinywa maji vile vile utapunguza njaa. Wataalamu wa lishe wanasema maji ni kirekebisho cha hamu ya kula ambacho unatakiwa unywe kabla ya kula ili usije vimbiwa kwa kula zaidi. Hivyo utajikuta njaa imepungua. Maji hayo pia ni dawa kwa waliozidiwa na uzito mwili (overweight) maana yanayeyusha mafuta yaliyozidi na kuyatoa kwa mkojo na jasho na kukupunguzia uzito kila siku.
Maji ni tiba binafsi (pocket doctor) pale unapo banwa na mawazo labda umechacha, bosi mkali, biashara imedoda, mwandani anasumbua kichwa chako n.k. kunywa maji mengi kukupunguzia mzigo huo wa mawazo na hakika utaukubali mpango huu. Maji humfanya binadamu aonekane kama mmea ulioota kando ya mto na asiyekunywa huonekana kama mmea uliooteshwa juu ya kichuguu! Wazee, Hakika ujana unarudi. Akina mama, mtaungua sana na hayo madawa ya kemikali kwa kutojua tu. Maji yanafanya kazi kushinda krimu au losheni yoyote ile duniani! Hata mimi natafuta mchumba anayekunywa maji walau glasi sita kwa siku, na nikimtazama kwa macho ajae katika mizani. Anayetaka kuamini aanze kunywa glasi nane tu kwa siku halafu baada ya wiki mbili aone maajabu.
Maji kwa wafanyakazi. Wewe kama ni mfanyakazi bila kujali ni wa sekta gani, jenga tabia ya kunywa maji glasi moja kila baada ya saa moja halafu baada ya majuma mawili tu utanipigia ukikiri ulivyonufaika. Maji yanakufanya uwe mjanja. Kwa kuwa yanamiliki 90% ya ubongo basi mtu asiyekunywa maji ni rahisi kudanganywa, kutapeliwa, kuzubaa, kutoeleweka maamuzi yako n.k. Maji kwa kuwa yanajaa mwilini kukupa afya na nguvu, basi anayekunywa maji si mwoga! Ni mtu anayejiamini na ni mshindi kwa wasiokunywa maji popote: darasani, kazini, biashara, shambani, michezoni n.k. Lakini ukinywa maji, huumwi hovyo! Amini msomaji wangu, wakati nakupa simulizi hii tamu malaika wa heri mbinguni wanapiga vinanda kuisifia nguvu hii kuu ya uumbaji duniani ambako pia Wataalamu wa afya duniani kote wameshikana mikono wakiirusha juu na kusema "REFUSHA, FURAHIA MAISHA KWA MAJI"
John Haule ni mpelelezi binafsi (Private investigator) anayejihusisha na tafiti zenye suluhisho kwa matatizo ya kijamii. Unaweza kumpigia kwa miadi ya ushauri juu ya tatizo lolote linalokusumbua kibinadamu. Anapatikana Car Painters - Temeke Stereo, Sandawe Street, jirani na Dr. Massawe. Simu: 0768 215 956 au email rumoursafrica@gmail.com

1 comments: